Thursday, August 21, 2014

SERENGETI INA TEMBO NA NYATI WENGI KULIKO MASAI MARA


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalando, amezindua taarifa ya takwimu ya sensa ya Tembo na Nyati kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti, (SENAPA) na Masai Mara ya nchini Kenya ikionyesha jumla ya tembo 192 wameuawa katika kipindi cha miezi 18.

 

Aidha, idadi Tembo walio kwenye hifadhi hizo ni 7,535 huku nyati wakiwa 61,896  ambapo  idadi kubwa ya wanyama hao wako kwenye hifadhi ya Serengeti yenye tembo  6,875 na Nyati 55,402 huku ile ya Masai Mara ikiwa na tembo 1,440 na Nyati 6,494.

 

Pia, zoezi la sensa la kuhesabu wanyama wote wakubwa nchini walio kwenye hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na mapori tengefu wakiwemo Tembo inaendelea na shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo desemba 30, mwaka huu.

 

Waziri Nyalando aliyasema hayo wakati wa uzinduzi huo ulifanyika jana Arusha  ambapo zoezi la ukusanyaji wa takwimu hizo uliyofanyika kwa wiki tatu kuanzia Mei 19, mpaka Juni 6, mwaka huu ikishirikisha wataalamu toka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Nchini, (TAWIRI) na Idara ya Utafiti wa Wanyamapori Kenya, (KWS).

 

Alisema kuwa hifadhi za Serengeti na Masai Mara zinategemeana kutokana na wanyama kuhama kutoka upande mmoja kwenda mwingine kwa vipindi mbalimbali vya mwaka  hivyo ili kufanikisha shughuli za uhifadhi hakuna budi kuboresha ushirikiano zaidi jambo litakalosaidia hata kukabiliana na majangili.

 

"Wataalam wetu hawa wamekuta mizoga ya tembo 192, kati ya hiyo 75 ilikuwa Serengeti (Tanzania) na mizogo 117 ikiwa Mara (Kenya), kati ya hiyo mizoga 13 ilikuwa ni ya tembo wenye umri mdogo," alisema Waziri huyo wa Maliasili na Utalii.

 

Aliwataka jamii na wanaharakati wa uhifadhi wa wanyamapori kutumia takwimu sahihi na za kisayansi katika kuelezea adhari za ujangili nchini huku akirejea takwimu mbalimbali zinazotolewa huku nyingine zikionyesha jumla ya tembo 10,000 huuawa kila mwaka nchini jambo alilodai kuwa kama zingekuwa sahihi basi kwenye utafiti huu wangekuta miziga si chini ya 5,000 .

 

 

Alisema kuwa shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na ufugaji kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi ya SENAPA , Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCAA) na Masai Mara ya nchini Kenya imekuwa ni changamoto kubwa katika suala zima la uhifadhi.

 

Kwa upande wake Mkurugezi wa KWS, Charles Musyoki, alisema kuwa kwenye sensa hiyo imeonyesha idadi ya tembo walio Mara ni ndogo ukilinganisha na wale walio Mara kutokana na wanyama hao huishi kuwa mzunguko kulingana na majira ya mwaka.

 

"Tunataka ushirikiano huu uendelee kwenye kukabiliana na majangili wa wanyamapori, hatutaki majangili watawale kwenye hifadhi zetu, hili tutalifanya kwa kuhakikisha askari wa wanyamapori wa hifadhi hizi mbili wanafanya kazi kwa pamoja," alisema Musyoki.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Simon Mduma, alisema kuwa sense hiyo iliyodhaminiwa na Taasisi ya Paul Allen umegharimu dola za Marekani 150,000 (sawa na zaidi shilingi 240 milioni) .

 

"Sensa hii imetumia fedha nyingi lakini tumefanya zoezi hili kisayansi, tulikuwa tunatumia ndege, tulikuwa tunahesabu wanyama na kuwapiga picha, hii imetusaidia kujua maeneo yapi ujangili hufanyika kutokana na mizoga tuliyoibaini na maeneo yenye muingiliano wa shughuli za kijamii," alisema Mduma.

 

Idadi ya wanyamapori hao imeongezeka ikilinganishwa na sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 1986 ambapo Tembo walikuwa 2,058 na nyati 54,979.

No comments: