*Huacha nyayo ukiukanyaga na huyeyuka
mkononi ukiushika
*Ni eneo ‘Takatifu’ la ibada na
matambiko kwa Wamaasai
BONDE la Mamlaka ya hifadhi ya
Ngorongoro ni miongozi mwa vivutio vya kitalii vinavyoleta wageni nchini mamia
kwa maelfu kuja kujionea moja kati ya maajabu ya dunia.
Mchanga huu wa maajabu ambao ni matokeo
ya mlipuko wa volcano kwenye mlima Oldonyo Lengai unaaminika tayari umetembea
umbali wa Kilometa 8 ndani ya bonde la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Afisa Mhifadhi Mkuu wa maendeleo ya
Utalii ndani ya NCAA, Asantael Melita anasema hadi sasa mchanga huo wa maajabu
umetumia muda wa miaka 42 kukamilisha mwendo wa umbali huo.
“Mchanga huu unaaminika kuwa ni matokeo
ya mlipuko wa volcano kwenye mlima wa Oldonyo Lengai uliorushwa maeneo
karibu na mlima uliokuwa kwenye eneo la Kreta ya Ngorongoro karibia miaka 3,000
iliyopita lakini baadaye mlima huo ulizama na kutengeneza mbonde la
Ngorngoro maarufu kama Kreta tunalolishuhudia hivi sasa,” anasema Melita
Afisa Uhifadhi huyo aliwaambia wandishi
wa habari waliotembelea eneo hilo katika moja ya ziara zinazoandaliwa na
kuratibiwa na NCAA kwa lengo la kuwapa upeo mkubwa wa kuelewa vivutio
vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo kuwa inaaminika mchanga huo wenye nguvu
za uvutano ulianza safari yake katika muda usiojulikana kutokana na kutokuwepo
takwimu sahihi za safari hiyo kwa miaka ya nyuma .
Ziara ya mchanga huo kwa mujibu wa
Melita ulianza kupimwa rasmi mwaka 1969 ambapo vipimo vinaonyesha hutembea kwa
wastani wa kiliomita 0.19.
Mchanga huo hutembelea kwa kusukumwa na
upepo huku ukiwa umejikusanya pamoja bila kuacha mabaki nyuma kiasi kwamba mtu
mgeni hawezi kujua ulipokuwa kipindi kilichopita hadi aelezwe na wenyeji.
Kwa sasa muonekano wa mchangao huo ni
kama vile umetengeneza umbo la mlima wenye urefu wa mita 10 kwenda juu na upana
wa mita 100 sawa na uwanja wa mpira wa miguu.
Maajabu mengine ya mchanga huo ni
mabadiliko yanayotokea kipindi cha kiangazi na masika ambapo urefu wake hubadilika
hadi kufkia mita 17 wakati upana huwa mita 45.
“Kati
ya miaka ya 1970 na 1980 mchanga huu ukiwa katika umbo la mlima ulikuwa
ukielekea upande ilipo hifadhi ya Serengeti na pale kuna mto unaopitisa maji
hivyo mwaka 1991 mchanga huo ulipokuwa ukiukaribia mto huo tulianza kuumiza
vichwa tukihofia kuwa utazama mtoni na hivyo kuwa mwisho wake,” anasema Melita
Anase,a hofu hiyo iliyeyuka mwaka 2000
kipindi cha mvua za El Nino ambapo ghafla mchanga huo ulibadili uelekeo kwa
kuacha kwenda hifadhi ya Serengeti na badala yake kuchukua mkondo unaoelekea
eneo la Enduleni.
Kwa mujibu wa vipimo vya kitaalamu,
inaaminika hivi sasa mchanga huo unaelekea kwenye milima ya Ngorongoro upande
wa mkoa wa Shinyanga ambapo ni eneo salama.
Hata hivyo kwa mujibu wa Melita, hivi
sasa mchanga huo umegawanyika katika makundi mawili tofauti, moja ambalo ndilo
kundi kunwa unaelekea milima ya Ngorongoro wakati ule mdogo bado unachukua
mkondo unaoaminika kuelekea hifadhi ya Serengeti.
Maajabu mengine yanayoambata na mchanga
huo ni kitendo cha mimea yote iliyo katika mkondo unakoelekea kukauka kabla
hazijafikiwa lakini mara baada ya mchanga kupita eneo hilo hupata rutuba
inayostawisha mimea mipya na hivyo kurejesha uoto wa asili ndani ya Kreta.
Melita anasema kuwa hakuna utafiti
uliofanyika mpaka sasa kubaini sababu ya maeneo yaliyopita mchanga huo kukauka
huku maeneo hayo yakionekana kuwa na rutuba baada ya kipindi kirefu kupita na
majani kuanza kuchipua upya .
Kutokana na maajabu ya mchanga huo,
nadhani kuna haja ya mamlaka husika kubadili namna na mfumo wa kuutangaza
kutokana na kutofahamika sana miongoni mwa wageni wanaotembelea hifadhi ya
Ngorongoro nikiwemo mimi mwenyewe ambaye awali sikuvutiwa sana kwenda
kuutembelea hadi nilipofika na kujikuta nikiushangaa mlima mzuri uliotengenezwa
kwa mchanga mweusi kabla kujulishwa kwa huo ndio mchanga wenyewe unaotembea.
Mvuto unaopatikana kwa yeyote anayefika
eneo hilo ndilo lilinifanya kuwa mtu wa kwanza kukimbilia kuushika mikononi
mchnaga huo lakini nikakumbana na maajabu mengine kwani ukiushikilia kwa muda
mikononi mchnagao huo huishia na utajikuta huna kitu mkononi.
Mlima huo unaotengenezwa na mchanga
laini hunavutia kila unapopiga hatua kuukwea kwani huacha alama za hatua
unazopiga lakini ukibahatika sehemu ya mchanga kuingia ndani ya viatu vyako
utajikuta ukikumbana na maajabu mengine kwani michanga hiyo hutoka yenyewe huku
miguu yako ikibaki safi kana kwamba umejipangusa na kitambaa.
Nadhani muda sasa umefika kwa maelezo ya
eneo hilo lenye upepo mkali lakini usiochukiza kutokana na mvuto wa mandhari
yake ubadilishwe na kuitwa mlima unaotembea badala mchanga unaotembelea.
Jina hili siyo tu kwamba utaelezea
uhalisia wa jambo lenyewe kutokana na mchanga huo kutengeneza kijimlima lakini
pia utavutia watu kutoka ndani na nje ya nchi kwenda kuutembelea mlima
unaotembe.
Pamoja na maajabu hayo ya kisayansi,
lakini kuna sayansi nyingine ya kijadi kwa watu wa jamii ya wafugaji wa
Kimaasai ambao wanaamini mchnaga/mlima huo una nguvu ya uponyaji na utatuzi wa
matatizo mbalimbali ikwemo upatikanaji wa mimba kwa wanawake wenye tatizo ka
kutopata watoto.
“Wamaasai wanaamini eneo ulipo mchanga
huo ni patakatifu hivyo huenda hapo na maziwa na kufanya tambiko yao ya kijadi
na wana fanikiwa kwenye yale wanayoyaomba kutokana na imani zao,” anasema
Melita
Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa
NCAA, Adam Akyoo, watu wengi hasa watalii wamekuwa na shauku ya kujua
nini mwisho wa safari ya mchanga huo mwepesi wenye rangi nyeusi ambao hata
ukiushika mkononi hutoweka na kurejea ulipoutoa baada ya muda mfupi.
Akyoo aliyekuwa ameongozana na waandishi
waliotembelea hifadhi hiyo alikiri hoja kuwa mchanga huo haujatangwa vya
kutosha kwa sababu siku za nyuma milima ulipo mchanga unaotembea ulikuwa
kwenye maeneo ya mambo ya kale na hivyo NCAA hawakuwa na mamlaka ya kuutangaza
hadi pale ulipoingia kwenye eneo la Mamlaka ndipo walipoanza kuutangaza kote
duniani na watu kuanza kumiminika kuja kuutembelea.
Meneja Uhusiano huyo anabainisha kuwa
NCAA wanatarajia wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi watamiminika
kutembelea mchanga huo kutokana na muitiko unaoapatikana kila wanapoelezwa
maajabu hayo. Nadhani huu ni muda sasa kwa watanzania wengi kutembelea Mamlaka
ya hifadhi ya Ngorongoro kushuhudia maajabu haya badala ya kubaki wasikilizaji
na kuacha wageni wakifaidi urithi huu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu.
No comments:
Post a Comment