MIRADI ya Ujirani mwema
inayotekelezwa na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, (KINAPA) kwa kiwango
kikubwa imekuwa chachu ya kuwaletea hamasa wananchi wanaoishi kuzunguka mlima kushiriki
kuulinda mlima huo kwa kutunza mazingira
yanayozunguka mlima huo.
Mkuu wa Hifadhi ya Kinapa, Etastus
Lufungulo anasema kuwa wametumia zaidi ya sh milioni 937 kwa kipindi cha miaka
mitano kusaidia miradi mbalimbali
iliyoibuliwa na wananchi wanaoishi maeneo kuzunguka mlima huo mrefu kuliko yote
barani Afrika.
Anasema kuwa fedha hizo
zilitolewa kuanzia mwaka wa fedha 2007/2008 mpaka mwaka huu wa fedha ambapo Sera
ya Ujirani mwema inataka wananchi husika
kupitia vikao vyao vya kijiji kuibua mradi na kuanza kuchangia angalau asilimia
30 ambapo Kinapa huchangia asilimia 70 iliyobaki.
Lufungulo anasema kuwa
miradi hiyo imetekelezwa kwenye wilaya za Rombo, Moshi, Siha, Hai na Longido ambapo miradi mingi ilikuwa
kwenye sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, mabwalo ya
kulia chakula, mabweni, vyumba vya maabara, vyoo na ununuzi wa samani.
Aidha kupitia mpango huo wa
ujirani mwema, Kinapa imesaidia uanzishwaji na ukarabati wa miradi wa miradi ya
maji, vitalu vya miti ambayo hutumiwa na wananchi kama kitega uchumi kwa
kuwapatia kipato kwani miti hiyo huuzwa kwa ajili ya kupandwa kwenye maeneo
mbalimbali yanayozunguka mlima huo kwa lengo la kuboresha na kutunza mazingira
ya mlima huo unaoliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni kutokana na kutembelewa
na idadi kubwa ya watalii kila mwaka.
“Tunapiga vita watu kukata
miti na majani msituni, hiyo ni agenda yetu kuu kwenye vikao vya Maendeleo ya kijiji,
tunahamasisha upandaji miti kwa wingi, kama ambavyo mnaona wenyewe namna watu walivyohamasika
kupandanda miti kwenye makazi yao”
“Hapa tumetoa elimu ya
mazingira kwa wananchi juu ya umuhimu ya kuulinda na kuutunza mlima wetu,
(Kilimanjaro) na imeeleweka ndiyo maana hata katika kutembea kwenu hapa
kijijini, mmeshuhudia namna mazingira
yalivyo mazuri kila nyumba watu wamepanda miti ya kutosha”
KATIBU wa Mradi mradi wa
maji wa vijiji vya Ashira na Samanga, Robert Mushi akitoa maelezo kwa jopo la waandishi wa
habari (hawapo pichani) juu ya uteklelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa Kinapa
nyumba ni tanki la maji.
Hiyo ni kauli ya Mweka
Hazina wa Mradi wa Maji wa vijiji vya Shira na Samanga, Amani Shao,
unaotekelezwa na wananchi kwa ufadhili wa zaidi ya asilimia 75 wa Kinapa kupitia
mpango wake wa Ujirani Mwema.
Anasema kuwa mabadiliko ya
fikra za wakazi wa maeneo hayo hasa kuhusiana na suala zima la utunzaji
mazingira umechangiwa na elimu ya mazingira waliyoipata lakini kikubwa zaidi ni
namna wanavyonufaika na mapato ya mlima Kilimanjaro kwa kusaidiwa kutekeleza
miradi kwenye maeneo yao.
“Unajua kwenye ujenzi wa
mradi huu wa maji awamu ya kwanza tuliifanya wenyewe mpaka kukamilika ambapo
ilituchukua muda mrefu kwani ilikuwa inatulazimu kuchangishana sisi wenyewe”.
“Lakini ilipofika awamu ya
pili Kinapa walijitokeza kutuunga mkono na kutusaidia fedha kiasi zaidi ya sh
milioni 36.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa jambo lililosaidia mradi huu kwenda
kwa kasi zaidi na wananchi kupata unafuu mkubwa,” anasema Shao.
Anasema kuwa pia wananchi
wanachangia nguvu kazi kwa kuchimba mitaro inayotumika kulaza mabomba hayo kwa
ajili ya kupeleka maji kwa nyumba za wanavijijii.
Afisa Mtendaji wa kijiji
cha Ashira, Vicky Lyimo anasema kuwa
mwaka jana pekee wamefanikiwa kupanda miti 4,000 kwenye eneo la nusu maili la
msitu wa mlima Kilimanjaro ambapo mwaka huu wanatazamia kupanda idadi hiyohiyo
ya miti au itaongezeka kidogo.
Akifafanua suala hilo mweka hazina wa mradi huo wa maji , Shao anasema
kuwa idadi hiyo ya miti haihusishi ile
inayopandwa na wananchi kwenye maeneo wanayoishi.
Anasema kuwa wananchi wengi
kwa sasa wanajitahidi kujiepusha na matumizi makubwa ya kuni kwa ajili kupikia
ambapo wengi wanatumia majiko banifu ambayo hayatumii nishati kubwa ya kuni au
mkaa kwa ajili ya mapishi ya vyuakula majumbani.
Kwenye mradi huo mbali na Kinapa
kupitia mpango wake wa ujirani mwema kuchangia kiasi hicho cha fedha kwa ajili
ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo kwa kujenga kisima chenye uwezo wa
kuhifadhi maji yenye lita za ujazo 150,000 wananchi nao wanachangia nguvu kazi
inayokadiriwa kuwa sawa na zaidi ya sh milioni 14.4 .
Mradi huo ukikamilika
unatarajia kuwanufaisha wananchi zaidi ya 1,500 wa vijiji hivyo viwili kwa
kuwapatia maji safi na salama yatakayofika kwenye maeneo yao kupitia mabomba.
Katibu wa Mradi huo, Robert
Mushi anasema kuwa mradi huo ulianza 2004 kwa wananchi kuchangishana ambapo
waliweza kutengeneza eneo la kuchukulia maji (intake) ambapo kutokana na
uwezo mdogo wa kifedha waliokuwa nao hatua
hiyo ilichukua muda mrefu mapka kukamilika.
Anasema kuwa mwaka 2011
wakiwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi huo ndipo Kinapa walianza kuwawezesha
jambo lililoongeza kasi ya mradi huo kwani waliweza kujenga kisima hicho
ambacho kimeshakamilika ndipo wakaanza awamu ya tatu ya kusambaza mambomba kwa
ajili ya kupeleka maji kwenye nyumba za wanavijiji wa Ashira na Samnaga.
“KINAPA wametupa vifaa vya
ujenzi kwa awamu ya tatu ya ujenzi ikiwemo mabomba yenye urefu wa mita 1,500,
hii kazi ya kusambaza mabomba tulitarajia ingekuwa imekamilika desemba mwaka
huu lakini tunakwamishwa na mawe ya pale
karibu na shule ya sekondari Ashira, kuna mawe mengi sana” anasema Mushi.
Anasema kuwa wanafanya kazi
ya kung’oa mabomba yaliyowekwa mwaka 1970 na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wa ambayo kwa
sasa hayakidhi haja kutokana na ongezeko kubwa la watu na mabomba hayo yamechakaa
kutokana na kutumika kwa muda mrefu.
“Unajua tuliamua kuanza
mradi huu baada ya maji kuwa kidogo, yakawa hayatoshelezi. Ilikuwa inalazimu
tuyatumie kwa mgao hivyo mwaka 2003 tukaanza kuchangishana na kuanza ujenzi wa
tanki lakuhifadhia maji mwaka 2005 ambalo
lilikamilika mwaka 2011” anasisitiza katibu huyo wa mradi.
Tanzania Daima pia ilifanikiwa kutembelea mradi wa ujenzi wa
bwalo la kulia chakula wanafunzi wa shule ya sekondari ya Olele iliyoko wilayani
Rombo unaofadhiliwa na Kinapa kupitia program yake ya ujirani mwema.
Bweni hilo lenye uwezo wa
kutumiwa na 120 kwa wakati mmoja limegharimu zaidi yash milioni 71 ambapo
Kinapa imechangia sh milioni 53 ikiwemo gharama za mafundi na vifaa.
MKUU
wa shule ya Sekondari
ya Olele, Bertha Hubert akimsikiliza diwani wa kata ya Olele, Michael
Mrema, (CCM), wakati akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) juu ya ujenzi wa bwalo la chakula
(linaloonekana nyuma) uliofadhiliwa na Kinapa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo
yenye jumla ya wanafunzi 441, Bertha
Hurbert anasema kuwa ujenzi wa bwalo hilo ulianza mwaka novemba 2009 ambapo
limekamilika mwanzoni mwa mwaka huu.
Anasema kuwa kwa sasa
wanafunzi wanatumia bwalo hilo kwa ajili ya kufanya mitihani ya Taifa ikiwemo
ile ya kidato cha pili na nne ingawa baadaye linatarajiwa kutumika pia kwa
shughuli za jamii pale litakapohitajika.
Diwani wa kata hiyo ya
Olele, Michael Mrema, (CCM) anasema kuwa michango kama hiyo inayotolewa na
Kinapa imekuwa chachu kubwa kwa wananchi
kuhamasika kutunza na kulinda mazingira.
“Kwa kweli kwenye kata yetu
vijana wamehamasika sana kutunza mazingira, hata moto ukitokea huko kwenye
msitu wa mlima Kilimanjaro wao wanajitolea kuuzima bila kutegemea malipo
yoyote” anasema Mrema.
Anasema kuwa hiyo
imechangiwa na ufadhili unaotolewa na Kinapa kusaidia miradi kama hiyo ya
ujenzi wa bweni ambayo wanakijiji walipaswa kuchangishwa ili iweze kutekelezwa
jambo ambalo lingewachukua muda mrefu na
wangesukumana hasa kutokana na ugumu wa maisha kwa sasa.
“Hapa wananchi wamehamasika
kuhusiana na masuala ya mazingira kiasi kwamba akitokea mtu anafanya uharibifu
wowote pengine wa kukata miti wanakijiji wenyewe wanatoa taarifa kwenye ofisi
ya kijiji” anasisitiza diwani Mrema.
No comments:
Post a Comment